Na Mwandishi Maalumu
SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili ya Hazina, imeipongeza Benki ya NBC kwa mafanikio makubwa ya kibiashara katika mwaka 2022 ambayo yameifanya itoe gawio la Sh bilioni 6 kwa Serikali.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu aliyasema hayo leo alipokuwa anapokea gawio hilo, huku akisisitiza kuwa, Serikali yenye hisa asilimia 30 katika Benki ya NBC inafurahia kuona mafanikio katika uwekezaji wake.
“Nimefarijika sana kusimama mahali hapa ili kupokea gawio la Serikali la Shilingi bilioni Sita (6). Kwa hili NBC mnastahili pongezi kwa kazi nzuri sana. Natamani kiwango kizidi kuwa kikubwa, mwaka jana mlitoa Shilingi bilioni 4.5 na nikiangalia miaka mitano iliyopita mlikuwa mnatoa wastani wa bilioni 1.2, mnafanya kazi nzuri sana. Hongereni,” alisema Mchechu.
Aliongeza kuwa, mwelekeo wa NBC katika mafanikio ndiyo matarajio ya Serikali ya kutaka kuona uwekezaji wa Serikali katika Taasisi na Mashirika ya Umma unaleta tija katika kuchangia mapato katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Alisema pamoja na pongezi hizo, anaamini benki inaweza kufanya mambo makubwa zaidi katika utendaji wake kwa kuongeza ubunifu na hivyo kutoa gawio kubwa zaidi kwa wanahisa wake.
“Naomba niwape challenge hiyo, kipindi kama hiki mwakani wanahisa wapate mara zaidi ya gawio la leo… najua mnaweza!,” alisema na kuongeza kuwa, fedha zilizopokelewa zitakuwa na mchango mkubwa katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya taifa ikiwemo kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za kijamii.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NBC, Dk. Elirehema Doriye, anafurahi kuona mafanikio ya benki yake, akisema ushahidi ni ongezeko la faida kabla ya kodi ya Sh bilioni 81.9 kwa mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 36. Mwaka 2021, benki ilipata faida ya Sh bilioni 60.
“Ndiyo maana tunafurahia kuipa Serikali gawio hili la Sh bilioni 6. Tunaamini kesho yetu itakuwa njema zaidi kwani Serikali inatupatia ushirikiano mkubwa, kuanzia kwako wewe Msajili wa Hazina na ofisi yako, Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Fedha na Mipango, lakini pia Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi Pamoja na kuweka vyema mchanganuo wa mafanikio ikiwa ni pamoja na mapato tangu kuanzishwa kwake hadi mwaka 2022, alisema wanatarajio makubwa zaidi kwa kuwa Serikali inazidi kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji nchini.
Ofisi ya Msajili wa Hazina ni msimamizi wa uwekezaji wa Serikali katika Taasisi, Mashirika ya Umma, Wakala za Serikali pamoja na Kampuni mbalimbali ambazo Serikali ina hisa chache, ikiwa na majukumu manne ambao ni pamoja na Kusimamia utendaji kazi wa Mashirika, Taasisi za Umma na Wakala za Serikali.
Majukumu mengine ni Kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu uwekezaji katika mitaji na usimamizi; Kuhifadhi kwa niaba ya Serikali rasilimali zilizowekezwa katika hisa na mali za Taasisi, Mashirika ya Umma, Wakala za Serikali pamoja na Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache; na Kusimamia urekebishaji na ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma pamoja na kufanya tathmini na ufuatiliaji.
Ends