Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Makamu wa Rais azitaka Taasisi za Umma kudhibiti mapato na ubadhirifu
24 Aug, 2025
Makamu wa Rais azitaka Taasisi za Umma kudhibiti mapato na ubadhirifu

Na Mwandishi wa OMH

 

 

Arusha. Taasisi za Umma zimetakiwa kuongeza nguvu katika kudhibiti upotevu na ubadhirifu wa rasilimali za umma.

 

 

Wito huo ulitolewa Jumapili, Agosti 24, 2025 jijini Arusha na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, wakati akifungua Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma.

 

 

“Pamoja na kuanzishwa kwa mifumo ya kukusanyia mapato kama GePG, TAUSI na usajili wa mashine za POS, bado kuna upotevu mkubwa wa fedha za Serikali, kama ambavyo ripoti za CAG za kila mwaka zinaonesha,” alisema katika mkutano uliowaleta pamoja washiriki zaidi ya 650.

 

 

Aliongeza: “Kwa muktadha huo, ninahimiza Taasisi na Mashirika ya Umma kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha; kudhibiti manunuzi na kuimarisha usimamizi wa mikataba; pamoja na kusimamia vyema rasilimaliwatu.”

 

 

Aidha, Mhe Mpango alisisitiza umuhimu wa kujenga ushirikiano wa kitaasisi kati ya mashirika ya umma ya Tanzania na yale ya kimataifa, ili kunufaika na masoko, teknolojia, tafiti, na hata utamaduni wa kazi.