Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Msajili wa Hazina afanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Lifezone Metal
02 Mar, 2026
Msajili wa Hazina afanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Lifezone Metal

Na Mwandishi wa OMH

 

Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amefanya mazungumzo na Bw. Keith Liddell, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa kampuni ya Lifezone Metals Limited, inayomiliki Tembo Nickel Corporation Limited kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina.

             

Mazungumzo hayo yalifanyika Jumatatu, Machi 2, 2026, katika Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, yakilenga kujadili maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Kabanga Nickel uliopo mkoani Kagera.

 

Mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya madini nchini, ukiwa na matarajio ya kuibadili Tanzania kuwa kitovu muhimu cha uzalishaji wa madini ya nickel duniani.

 

Mradi wa Kabanga unatarajiwa kuongeza thamani ya rasilimali za nickel kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa ya uchenjuaji, kukuza ajira kwa Watanzania, kuimarisha ujuzi wa ndani, na kuongeza mapato ya Serikali pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.

 

Ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji unaonesha dhamira ya kuendeleza rasilimali za nchi kwa manufaa mapana ya wananchi, sambamba na kuimarisha uwazi, uwajibikaji na tija katika usimamizi wa uwekezaji wa kimkakati.