Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Mashirika ya Umma muhimu kwa utalii wa matibabu
15 Aug, 2025
Mashirika ya Umma muhimu kwa utalii wa matibabu

Na mwandishi wa OMH

 

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina imesisitiza umuhimu wa mashirika ya umma katika kuhakikisha mafanikio ya utalii wa matibabu kwa kuboresha huduma za afya na miundombinu.

Kauli hiyo imetolewa na Bw. David Shambwe, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji wa Mashirika yasiyo ya Kibiashara, alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) yaliyofanyika leo, Agosti 15, 2025, katika Ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Bw. Shambwe amesema mashirika ya umma ni rasilimali za kimkakati kwa maendeleo ya taifa katika sekta ya afya, kwa kuwa yanatoa huduma maalum na za kiwango cha juu ambazo pengine sekta binafsi pekee isingeweza kuzitoa.

Ameongeza kuwa mashirika hayo yamewekeza zaidi katika sekta ya afya, hivyo kuongeza uwezo wa nchi kutoa huduma za matibabu kwa viwango vya kimataifa.

Ameeleza kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikichangia katika kuboresha sekta ya afya kwa kuimarisha ubora wa huduma, uimara wa kiutendaji na ushindani kwa kuweka misingi ya utawala bora, uimara wa kifedha, ufanisi wa uendeshaji, na maendeleo ya rasilimali watu.

Kwa mujibu wa Bw. Shambwe, uwekezaji na uboreshaji wa miundombinu katika sekta ya afya unaongeza uwezo wa Tanzania kuhudumia wagonjwa wa ndani na wale wanaotoka nje ya nchi, hali inayochochea ukuaji wa utalii wa matibabu.