SERIKALI imekabidhi uangalizi wa mali zote zilizopo katika shamba la ngano la Basotu wilayani Hanang kwa halmashauri ya wilaya hiyo mpaka hapo yatakapotolewa maelekezo mengine.

Hatua hiyo imekuja baada ya mali katika shamba hilo kuwa chini ya uangalizi wa Mfilisi, Kampuni ya Uwakili ya Tadayo kwa zaidi ya miaka 15. Awali, mfilisi chini ya Wakili Joseph Tadayo, Mbunge wa sasa wa Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro, alikabidhiwa kwa ajili ya kuuza shamba na mali zake, lakini baadaye serikali ilisitisha uamuzi huo.

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto jana alipokea mali za shamba hilo la Basotu kutoka kwa Mfilisi, makabidhiano yaliyofanyika katika Ofisi za Msajili wa Hazina, jijini Dar es Salaam.

“Ofisi yangu inashukuru kwa kazi ya uangalizi iliyofanywa na Kampuni ya Tadayo licha ya kuwepo kwa changamoyo kadhaa,” alisema Msajili wa Hazina mara baada ya kupokea hati ya makabidhiano.

Hati hizo zinaonesha kuwepo kwa mali mbalimbali katika shambali hilo lenye ukubwa wa hekta 5,138 ikijumuisha na majengo 37, zikiwemo nyumba za makazi 28, maghala mawili, vihenge (silos) sita, ukumbi wa starehe, mgahawa, kanisa, duka na mitambo mbalimbali pamoja na matrekta na mashine za kuvunia nafaka.

 

Mara baada ya kukabidhiwa hati za mali ya shamba hilo, Mgonya alizikabidhi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hanang, Jenifa Omolo kwa ajili ya uangalizi.

“Kwa upande wa Halmashauri, Ofisi yangu inashukuru uongozi wa Halmashauri kwa ushirikiano mkubwa ambapo imekuwa ikitupatia na leo hii tunaiongezea jukumu lingine na uangalizi wa mali mpaka hapo maelekezo mengine ya Serikali yatakapotolewa,” alisema Mgonya, huku Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hanang akiahidi kutimiza wajibu wake ili kulinda mali hizo za Serikali.

 

Naye Tadayo, alisema amekuwa mwenye furaha kukabidhi mali hizo, baada ya kuwa mwangalizi kwa muda mrefu, huku akikabiliana na changamoto kadhaa.

 

Shamba la Bassotu ni kati ya mashamba saba ya ngano ya Serikali wilayani Hanang yaliyokuwa chini ya Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (NAFCO) Aidha ni Shamba pekee ambalo halikubinafsishwa baada ya Serikali kusitisha uamuzi huo mwaka 2007. Kutokana na kukaa muda mrefu bila kubinafsishwa, kuliibuka vitendo vya uvamizi kutoka kwa wakulima na wafugaji, hali iliyoilazimu Halmashauri kuomba shamba hilo liwekwe chini ya usimamizi wao ili Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa lengo la vitendo vya uvamizi wa shamba na wizi wa mali.

Mashamba mengine ni Gawal, Warret, Gidagamowd, Satchet, Murjanda na Mulbadaw. Mashamba ya Gawal na Warret yalikabidhiwa kwa Halmashauri ya wilaya na kugawiwa wananchi kwa matumizi ya kilimo, ufugaji na makazi, na mashamba ya Gidagamowd, Satchet na Murjanda yalibinafsishwa kwa Kampuni ya Ngano Limited mwaka 2005. Shamba la Mulbadaw liliuzwa kwa Haydom Lutheran Hospital mwaka 2006.

 

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&ENDS&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&