Na Mwandishi Maalumu, Dodoma

Ni gawio la kihistoria! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel – Tanzania kuilipa Serikali ya Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 32.9 kama gawio na michango maalumu ya maendeleo kutokana na faida yake ya mapato katika Mwaka wa Fedha 2019/20.

 

Ni historia kwa kuwa kabla ya gawio la mwaka huu, Airtel iliyo katika uhusiano wa kibiashara na Serikali tangu mwaka 2001, ilitoa gawio mara moja tu la shilingi bilioni 3.2 katika mwaka 2007/8, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kuendeshwa kwa hasara.

 

Hata hivyo, tangu pande hizi mbili zilipoingia katika makubaliano maalumu ya kiutendaji na kiumiliki kuanzia mwezi Juni 2019, ufanisi wa kiutendaji umepaa, na ndiyo maana Serikali yenye hisa asilimia 49, kwa mara ya kwanza, imevuna faida nono ya uwekezaji ndani ya Airtel.

 

Mfano wa hundi mbili za fedha hizo kutoka Airtel ziliwasilishwa hivi karibuni Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Airtel – Tanzania, Gabriel Malata na kupokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, ambaye pia ni mlipaji Mkuu wa Serikali, Doto James huku akishuhudiwa na Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka ambaye Ofisi yake inasimamia uwekezaji wa Serikali katika mashirika, taasisi, na makampuni ya umma ambayo serikali ina hisa.

 

Akikabidhi hundi hiyo, Malata alisema katika kiwango hicho cha shilingi bilioni 32.99, shilingi bilioni 18.99 ni gawio, na shilingi bilioni 14 ni mchango maalumu wa maendeleo kwa Serikali baada ya Kampuni hiyo kupata faida ya bilioni 38.5 kwa mwaka unaoishia Desemba 2019/2020.

 

Akielezea mafanikio yaliyowezesha Kampuni yake kutoa gawio nono na michango ya maendeleo ya shilingi bilioni 1 kila mwezi, Malata alisema licha ya uwekezaji mzuri katika upanuzi wa mtandao, idadi ya wateja imeongezeka kutoka milioni 11.4 mwezi Machi 2019 hadi milioni 13.3 mwezi Machi 2020; na kwa sasa, umiliki wa soko ni asilimia 27, kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

 

Aliongeza kuwa Airtel – Tanzania imetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 500 huku wafanyakazi wa kigeni wakiwa saba tu na kupitia Airtel, Watanzania 350,000 wamejiajiri kwa kuuza bidhaa na huduma za Kampuni ya Airtel – Tanzania kama vile vocha na uwakala wa Airtel Money hivyo kuchangia maendeleo ya uchumi kwa kulipa ushuru kwa Serikali

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, James alisema tukio la Airtel la kutoa gawio na mchango wa maendeleo wa shilingi bilioni 32.99 ni la kihistoria.

 

“Hii ni siku nzuri sana kwangu ninaposikia taasisi ambazo Serikali imewekeza  hisa zinafanya vizuri na kulipa gawio kwa Serikali kutokana na uwekezaji uliofanyika. Kiasi hiki cha gawio cha Shilingi bilioni 18.9 kinachotolewa na Airtel kwa mwaka 2019/20 ni kikubwa na kitasaidia sana katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ya nchi.

 

“Nimefahamishwa kuwa katika historia ya uwekezaji wa Serikali katika makampuni yenye uwekezaji wenye hisa chache (Minority Interest), kiasi hiki hakijawahi kufikiwa na mwekezaji yeyote. Hivyo, nipongeze juhudi za makusudi na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Raisi Dkt. John Pombe Joseph Mugufuli”, alisema James ambaye mara kwa mara aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa usimamizi mzuri wa mashirika na taasisi unaoendelea kuinufaisha Serikali kupitia ufanisi katika uwekezaji wake.

 

Aliongeza kuwa haikuwa kazi nyepesi kwa Serikali kuongeza hisa zake kutoka asilimia 40 hadi 49, na haikuwa rahisi kuishawishi Airtel kuridhia kumwaga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa Serikali kila mwezi kuanzia mwaka jana.

 

Kutokana na mafanikio haya ya Airtel, Katibu Mkuu ameyataka makampuni na mashirika mengine ambayo Serikali inamiliki hisa kuongeza ufanisi ili yaweze kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya nchi ikiwemo kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii kama vile afya, elimu, na maji kwa Watanzania wote. Akisisitiza hili James alisema:

 

“Mashirika ya umma na makampuni ambayo bado yanatoa gawio dogo na yale ambayo hayatoi gawio yanatakiwa kujitathmini na kuhakikisha yanafanya vizuri na kulipa gawio ili kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo”.

 

Naye Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema Ofisi yake imeendelea kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha taasisi, mashirika ya umma na makampuni ambayo Serikali ina hisa yanaendeshwa kwa tija ili yaweze kutoa gawio endelevu kwa Serikali.

 

Ndani ya miaka mitano ya utawala wa Raisi Magufuli, ufanisi katika uwekezaji wa Serikali katika mashirika ya umma, taasisi na makampuni ambayo Serikali ina hisa chache umepaa na kuiwezesha Serikali kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 161 mwaka 2014/15 hadi shilingi trilioni 1.05 katika Mwaka wa Fedha 2018/19.

 

“Na leo hii, hizi shilingi bilioni 32.99 za gawio na michango kutoka Airtel si ndogo. Ukitaka uijue si ndogo, chukua bilioni 32.99, chukua wastani wa kituo cha kisasa cha afya ambacho kila kimoja kinagharimu kati ya shilingi milioni 400 na 500, gawanya utaweza kuona ni vituo vingapi vinaweza kujengwa. Chukua hivyo hivyo katika maeneo mengine kama elimu na kadhalika,” alisema Mbuttuka katika kuonyesha thamani ya gawio na michango inayokwenda Serikalini kutoka katika uwekezaji wake.

 

Aliongeza kuwa, licha ya ufanisi wa kimapato, pia kumekuwa na makerekebisho makubwa yaliyofanyika katika mashirika ya umma, ikiwa ni pamoja na kuimafrisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielekitroniki, kuimarisha bodi za wakurugenzi, udhibiti wa matumizi, na kuongeza usimamizi wa makampuni yanayomilikiwa kwa hisa chache.

 

Airtel imekuwa taasisi ya tatu kuipa gawio Serikali ndani ya mwezi mmoja, kwani mwezi Agosti 10 mwaka huu, Benki ya CRDB ilitoa gawio maalumu la shilingi bilioni 9.3 kwa Serikali, ikafuatia na Benki ya NMB wiki moja baadaye ambayo ilitoa shilingi bilioni 15.2, hivyo kuifanya Serikali kuvuna takribani shilingi bilioni 58 katika kipindi hicho.

 

Mwisho