TAARIFA KWA UMMA

KIINI CHA UBORA WA OFISI YA MSAJILI WA HAZINA NA MATOKEO CHANYA KWA TAIFA NI SISI WATUMISHI WENYEWE – TR.

Msajili wa Hazina (TR), Ndg.Athumani Selemeni Mbuttuka amebainisha kuwa kiini cha ubora, weledi, ufanisi na matokeo chanya ya majukumu iliyokasimiwa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) anayoiongoza kama mtendaji mkuu pamoja na maboresho mengine zaidi yanayoendelea kufanyika ni watumishi wenyewe kila mmoja kwa nafasi yake na kada yake aliyoajiriwa nayo.

Ametanabaisha hili wakati mkutano wake na watumishi wote uliofanyika leo jijini Dar Es Salaam katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), mkutano uliolenga zaidi kujadiliana mambo mbalimbali ya mwenendo wa utekelezaji wa majukumu ya ofisi pamoja na uibuaji mbinu mbalimbali za utunzaji bora zaidi wa kumbukumbu na nyaraka za kikazi za ofisi.

“Ni lazima tujijengee tabia na mwenendo wa kujifunza, kudadisi na kufuatilia vitu kwa umakini mkubwa zaidi. Mnatambua fika kuwa dhima kuu ya Ofisi yetu ni utunzaji wa mali za Serikali hivyo tuna wajibu mkubwa pia wa kufanya kazi kwa karibu na kuwahudumia wadau na wateja wetu wote muhimu kwa maslahi mapana ya Ofisi na Taifa kwa ujumla hivyo kupiga vita adui ‘maslahi binafsi’.

Vilevile ameongezea kuwa, pamoja na changamoto ambazo zinashughulikiwa kwa kushirikiana na mamlaka nyinginezo za Serikali, watumishi wanapaswa kujituma na kuongeza ubunifu zaidi katika maeneo yao ya kazi na katika majukumu ya msingi akibainisha machache kwa mfano; mbinu za ukusanyaji fedha za Umma ili kukuza pato la Serikali na Taifa, ujirani zaidi katika kuzisimamia bodi na menejimenti za Taasisi na Mashirika ya Umma ili kufanya kazi vema zaidi na kuleta tija kwa Taifa.

Pia katika mkutano huo Msajili wa Hazina amewataka watumishi kuwa wawazi katika kuyasema mapungufu mbalimbali ya kiutendaji yanayoleteleza kuwapa changamoto katika utekelezaji wa kazi na majukumu kwa mujibu wa mpango kazi na mtiririko wa fedha kwa namna zinavyopatikana na kugawanywa ili kutimiza malengo ya Ofisi na Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujumla wake.

Nae Mwenyekiti wa TUGHE Ofisi ya Msajili wa Hazina Ndg.Hussein Kakurwa, akimshukuru Msajili wa Hazina kwa niaba ya watumishi wote; alimpongeza kwa uamuzi na hatua yake muhimu sana ya kuitisha mikutano ya mara kwa mara na watumishi wote kwani ni takwa la kisheria sehemu za kazi kwani inaibua hoja mbalimbali na kuleta tija katika utekelezaji na kuongeza kuwa watumishi wa OTR wanafarijika kwa hatua hiyo kwani wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanalinda mali za Serikali kwa uzalendo wa hali ya juu hali akiwakumbusha kuwa Serikali inawategemea na kuwaamini sana katika hilo.

Imetolewa na:

Gerard Julius Chami

Mkuu wa Kitengo

Uhusiano, Habari na Mawasiliano,

Ofisi ya Msajili wa Hazina,

DAR ES SALAAM.

18 Septemba, 2018.